Utangulizi
Ndoa ilianzishwa na Mungu katika Edeni na ikathibitishwa na Yesu kuwa muungano wa maisha yote kati mwanaume na mwanamke katika wenzi wa upendo. Kwa Mkristo kifungo cha ndoa ni kwa Mungu na pia kwa mwenzi, na wenzi wanaokishiriki sharti wawe wenye imani moja tu. Upendo wa hiari, heshima staha na wajibu ndiso nyuzi za uhusiano huu, ambao utaakisi upendo, utakatifu, ukaribu kudumu kwa uhusiano kati ya Kristo na Kanisa lake. Kuhusu talaka, Yesu alifundisha kwamba mtu amwachaye mwenzi wake isipokuwa kwa sababu ya uasherati, na kuoa au kuolewa na mwingine azini. Ingawa uhusiano wa baadhi ya familia fulani huenda ukashindwa kufikia lengo, wenzi wa ndoa ambao hujitoa kamili kila mmoja kwa mwenzake katika Kristo wanaweza kufikia umoja wa upendo kupitia uongozi wa Roho na malezi ya kanisa. Mungu hubariki familia na anakusudia kwamba jamaa katika familia watasaidiana wao kwa wao kufkia upevu kamili. Wazazi wawalee watoto wao kumpenda na kumtii BWANA. Kwa kielelezo chao na maneno yao wawafundishe kwamba Kristo ni mtiishaji mwenye upendo, daima mpole na mwenye kujali, ambaye anawataka wawe viungo vya mwili wake, familia ya Mungu. Kukuza uhusiano wa karibu katika familia ni mojawapo ya alama ya kujulisha ujumbe wa injili ya mwisho. (Mwa.2:18-25; Yoh.2:1-22; 2Kor.6:14; Efe.5:21-33; Mt.5:31, 32; Mk. 10:11, 12; Luk.16:18; 1Kor.7:10, 11; Kut.20:12; Efe.6:1-4; Kumb.6: 5-9; Mith. 22:6; Mal. 4: 5, 6)
Nyumbani ni mahali pa msingi pa kurejeza sura ya Mungu kwa wanaume na wanawake. Katika familia, baba, mama na watoto wanaweza kujieleza kikamilifu, wakitimiza mahitaji yao ya kuhusiana, kupendana na kuthaminiana. Nyumba pia ni mahali ambako neema ya Mungu, ile misingi ya kikristo inapofanyiwa mazoezi na thamani zake zikamishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Nyumbani ni mahali pa furaha kubwa. Vile vile nyumbani panaweza pakawa mahali pa maumivu makali. Maisha ya maelewano hudhihirisha misingi ya kikristo na kufunua tabia ya Mungu. Bahati mbaya maisha ya namna hii ni magumu kupatikana kwenye nyumba nyingi. Badala yake kinachoonekana, ni maisha yenye kufunua mioyo ya kibinadamu iliyojaa ubinafsi – magomvi, uasi, ushindani, hasira, ubaya na hata ukatili. Haya hayakuwa sehemu ya mpango wa awali wa Mungu tangu awali. Yesu alisema, “tangu mwanzo haikuwa hivi.” (Mt.19:8)
Tangu Mwanzo
Sabato na ndoa ni karama mbili za asili za Mungu kwa mwanadamu. Zilikusudiwa kumfurahisha mwanadamu kwa kumpa mwanadamu pumziko na kuthaminiana. Vilikuwa ni viwili vilivyokamilisha kazi ya Mungu ya uumbaji na kuufanya uwe mwema sana. (Mwa.1:31). Kwa kuanzisha sabato, Mungu alimpa mwanadamu wakati wa kupumzika na kufanywa upya, wakati wa ushirika naye. Kwa kuunda familia ya kwanza, Mungu aliunda msingi wa kijamii, kuwapa ufahamu wa kuthaminiana na fursa ya kufanya huduma kwa Mungu na kwa wanadamu.
Mwanamume na Mwanamke kwa Mfano wa Mungu.
Mwanzo 1:26, 27 inasimulia uumbaji wa Mungu ambao ungekalia dunia. “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale … Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba mwanamume na mwanamke.” Siyo kwamba neno mtu linamaanisha mwanamume aliumbwa kwa sura ya Mungu, halafu Mwanamke akaumbwa kwa mfano wa mwanamume bali wote mwanaume na mwanamke waliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Kama ambavyo Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni Mungu, mwanamume na mwanamke ndio wanaofanya mtu. Kama Mungu, bado ni wamoja kwa asili, kwa tathmini, lakini siyo nafsi moja. (cf. Yoh.10:30; 1Kor. 11:3). Maumbile yao hujaliza upungufu wa upande mwingine na utendaji wake ni wa kushirikiana.
Jinsia zote mbili ni njema (Mwa.1:31) pamoja na majukumu yake kutofautiana. Familia na nyumba hujengwa kwa utofauti wa jinsia. Mungu angeweza kufanyiza namna tofauti ya kuzaana kama ilivyo kwa viumbe wengine. Ulimwengu wa jinsia moja peke yake hautakuwa mkamilifu. Kuridhika kwa kweli kunawezekana tu katika jamii ambayo inahusisha wa kiume na wa kike. Usawa siyo suala la kuuliza hapa kwa sababu jinsia zote ni muhimu.
Katika siku yake ya kwanza, Adamu, mzaliwa wa kwanza na hivyo kiongozi wa wanadamu wote, alijisikia tofauti, hapakuwa na wa kufanana naye (Mwa.2:20). Mungu aliliona hitaji hili na ndiyo maana akasema siyo vema mtu huyu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. (Mwa.2:18). Neno neged lililotumika hapa, lina maana ya kusimama kando au mbele ya, kuwa kinyume cha, kushabihiana ya moja au kitu. Kwa hiyo Mungu alimletea Adamu usingizi mzito, na akitumia ubavu wake moja, (Mwa.2:21, 22), alimtengenezea Adamu mwenzi wake. Alipozinduka kutoka usingizi wake, Adam mara moja alitambua uhusiano wa karibu ambao kitendo maalum cha uumbaji kimewezesha. Alisema kwa mshangao “sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. (Mwa.2:23 cf. 1Kor.11:8).
Ndoa.
Kutoka kwenye tofauti ya wanaume na wanawake, Mungu alileta utaratibu – umoja. Ijumaa ya kwanza, aliunda ndoa ya kwanza akiwaunganisha wawili kuwa moja. Na ndoa imekuwa msingi wa familia, msingi wa jamii tangu wakati huo. Biblia huizungumzia ndoa kuwa inatokana na uamuzi wa vipande viwili kuunganishwa na kuwa kitu kimoja. Mmoja “atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili moja.” (Mwa.2:24).
1. Kuacha.
Msingi muhimu kwa ndoa ni kuachana na mahusiano ya zamani. Mahusiano ya ndoa yanataka kuachana na mahusiano ya mzazi na mtoto wake. Kwa jinsi hiyo, kuwaacha wazazi, husaidia kuambatana na mwenzi katika mahusiano ya ndoa.
2. Kuambatana.
Neno la kiebrania lililotafsiriwa kuambatana linatokana na neno lenye maana ya kushikana, kufungamana, kuungana na kushikilia. Kama nomino, hutumika pia kwa kuchomelea “kuunga” (Isa.41:7). Ukaribu unaowasilishwa na neno hili, hutumika pia katika mahusiano kati ya Mungu na watu wake. “Mche BWANA, Mungu wako, umtumikie yeye; ambatana naye, na kuapa kwa jina lake.” (Kumb.10:20).
3. Kuweka agano.
Katika maandiko, ile ahadi ambayo waliooana wanapeana huitwa agano – makubaliano makini kwenye maandiko matakatifu. (Mal.2:14; Mith.2:16, 17). Mahusiano baina ya mume na mke yapaswa kufanana na agano la Mungu la milele na watu wake ulimwenguni – kanisa. (Efe.5:21-33). Kuahidiana kwao kwapaswa kuwa kwa uaminifu ambao unaakisi uaminifu wa Mungu (Zab.89:34; Omb. 3:23). Mungu, familia za wanaofunga ndoa, na jamii inashuhudia agano ambalo ni siri. Hapa kuna umoja katika maana halisi, wafunga ndoa wanatembea pamoja, wanasimama pamoja na kushiriki uhuasiano wa ndoa. Agano hilo linaridhiwa mbinguni. “Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.” (Mt.19:6). Wanandoa wakristo huamini kwamba wamepeana agano kuwa waaminifu kwa kila moja wao hadi kifo kitakapowatenganisha.
Kuwa mwili moja.
Kuacha na kufanya agano kuambatana hufanyiza mwungano ambao ni siri. Hapa ni umoja kwa maana kamili – waliofunga ndoa hutembea pamoja, husimama pamoja na kushiriki tendo la ndoa. Mwanzoni, jambo hili huhusu mwungano wa kimwili. Kadiri maisha ya pamoja yanavyoendelea, ndipo mwungano wa mawazo na hisia hushikamana kuongezea mwungano huu wa kimwili.
a) Kutembea pamoja.
Kuhusu mahusiano yake na wanadamu, Mungu anauliza “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? (Amo.3:3). Swali hilo pia ni muhimu kwa wanaokuwa mwili moja. Mungu alionya Israeli wasifunge ndoa na mataifa jirani kwa sababu wangewapotosha wana wao waabudu miungu mingine. (Kumb.7:4; cf. Yosh.23:11-13). Waisraeli walipopuuza maelekezo hayo, walipatilizwa (Amu.14:16; 1Falm.11:1-10; Ezr.9:10). Paulo anarudia kanuni hii kwa mapana yake kuwa “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani gani kati ya Kristo na Beliari? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? (2Kor.6:14-18).
Ni wazi Maandiko yamekusudia waumini wafunge ndoa na wamini wenzao tu. Lakini kanuni hii inavuka ng’ambo zaidi. Umoja wa ukweli hudai kupatana juu ya imani na matendo. Tofauti ya dini hufanya mtindo wa maisha wenye migogoro na kufanya nyufa kwenye ndoa. Kuepuka hayo, Maandiko hufundisha waumini kufunga ndoa katika jamii yao wenyewe.
b) Kusimama pamoja.
Kuwa mwili moja, wawili wapaswa kuwa na utii wa imani wa kila moja kwa mwenzake. Mtu anafunga ndoa hujitahatarisha kwa yale ambayo mwenzake anakuja nayo. Wanapofunga ndoa hutangaza ukubali wao kushiriki uwajibikaji wa wenzi wao, kusimama pamoja na washiriki wao dhidi ya kila jambo. Ndoa hutaka upendo wa daima usiokata tamaa. Watu wawili hushirikiana vyote walivyo navyo, siyo tu miili yao, siyo tu mali zao; bali pia mawazo yao na hisia zao, furaha zao na huzuni zao, matumaini yao, hofu zao, mafanikio yao pamoja na kushindwa kwao. Kuwa mwili moja humaanisha wawili wanakuwa na mwili moja kikamilifu, moyo na roho moja na bado wakabaki ni nafsi mbili tofauti.
c) Tendo la ndo.
Kuwa mwili moja huhusisha mwungano wa kijinsia. “Adam akamjua Hawa mkewe naye akapata mimba.”(Mwa.4:1). Katika msukumo wao wa kuunganishwa pamoja, msukumo ambao wanaume na wanawake wana hisia nao tangu siku za Adam na Hawa, kila ndoa inayo kisa chake cha mapenzi. Kitendo cha ndoa huelezea ukaribu uliopo kuliko chochote kuhusiana na mwungano wa mwili, kihisia na kiroho. Upendo wa ndoa wa kikristo wapaswa kuwa wenye joto, furaha na kufurahiana. (Mith.5:18, 19).
Ndoa na iheshimiwe na watu wote na malazi yawe safi” (Ebr.13:4). Maandiko huelezea kuwa kitendo cha ndoa baina ya mume na mke ni mpango wa Mungu. Ni kama mwandishi wa Waebrania asemavyo siyo najisi, siyo dhambi, siyo kitendo kichafu. Ni sehemu ya heshima kubwa kwenye ndoa – patakatifu pa patakatifu ambako mume na mke hukutana peke yao kushangilia upendo kila moja kwa mwenzake. Ni wakati ambao unapaswa kuwa mtakatifu na wenye msisimko unaofurahisha.
5. Upendo ki Biblia.
Upendo wa ndoa ni upendo usio na masharti, wenye hisia na kujitoa kimwili kila mwanandoa kwa mwenzake ambao hutengeneza mazingira ya kukua pamoja katika sura na mfano wa Mungu kwa hali zote, kimwili, kihisia, kiakili na kiroho. Aina tofauti za upendo hutenda kazi katika ndoa: kuna nyakati za hisia, kuhurumia na kufariji. Pia kuna nyakati za kumilikiana katika hali zote. Hata hivyo aina ya upendo unaodumu ni ule wa agape, yaani usio wa ubinafsi, usiojitumikia ambao hujenga msingi wa upendo wa ndoa unaodumu.
Yesu alidhihirisha upendo wa hali ya juu pale alipokubali kubeba hatia na matokeo ya dhambi zetu akaenda msalabani. “Naye amewapenda watu wake katika ulimwengu, naam aliwapenda upeo” (Yoh.13:1). Alitupenda sisi pamoja na matokeo ya dhambi zetu kwake. Huu ni upendo usio na masharti wa Yesu Kristo.
Akisimulia upendo huu, Paulo anasema “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu; bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. (1Kor.13:4-8).
Upendo wa agape umesimikwa kwenye chanzo cha milele na hutenda kazi mahali ambako aina zingine za upendo zitashindwa. Hupenda hata kama kuna ugumu kiasi gani. Pasipo kujali kwamba mwenzi hapendeki kiasi gani wenyewe bado huchanua tu. Ni mtazamo wa kiakili unaosimamia uamuzi wa nia.
6. Uwajibikaji binafsi kwa mambo ya kiroho.
Pamoja na wanandoa kujifunga kila moja kwa mwenzake kwa njia ya agano, kila mmoja anawajibika binafsi kwa maamuzi ayafanyayo. (2Kor.5:10). Kwa maana hiyo, mwenzi hatamlaumu mwenzake kwa makosa ambayo kayafanya binafsi. Pia wapaswa kuwajibikia ukuaji binafsi wa mambo ya kiroho; hakuna atakayetegemea ustawi wa kiroho wa mwenzake kupata nguvu za kiroho. Hata hivyo, ushirikiano wa mtu na Mungu utamsaidia mwingine kuwa chanzo cha kuimarika na kumtia moyo.
Matokeo ya Kuanguka kwenye Ndoa
Kuharibika kwa sura ya Mungu kulikoletwa na dhambi kumeathiri ndoa, kama ilivyotokea kwenye maeneo mengine ya uzoefu wa mwanadamu. Ubinafsi umeingilia mahali pa upendo mkamilifu ulikotawala. Ubinafsi ni kisababishi cha msingi cha wote wasiovutwa na upendo wa Kristo. Hupinga kujitoa, utumishi na kutoa kama injili inavyotaka, na huonekana kwenye kila anguko la kikristo.
Kwa kutokutii kwao, Adam na Hawa walivunja makusudi ya kuumbwa kwao. Kabla ya dhambi waliishi kwa uwazi mbele za Mungu. Baada ya dhambi, badala ya kumjia Mungu kwa furaha, walijificha kwa hofu na kujaribu kufunika ukweli unaowahusu na kukana kuwajibika kwao kwa matendo waliyofanya. Wakiwa wamegubikwa na hatia ya dhambi, hawakuweza kukutana na jicho la Mungu na la malaika watakatifu. Ukwepaji huu wa kuwajibika na kujihesabia haki kumekuwa tabia ya mwanadamu mdhambi mbele za Mungu. Hofu iliyowafanya kufunika walilotenda, haikuharibu tu uhusiano wa Adamu na Mungu bali pia mahusiano ya wanandoa. Mungu alipowahoji, kila moja alijaribu kujitetea kwa hasara ya mwingine. Hoja zao zilionyesha kuwa upendano uliowekwa na Mungu wakati wa uumbaji ulikuwa umetoweka.
Baada ya dhambi, Mungu alimwambia mwanamke, “tamaa yako itakuwa kwa mume wako naye atakutawala. (Mwa.3:16). Alikusudia kanuni hii pasipo kuondosha ule usawa waliokuwa nao, kuwafaidia wanandoa hawa na wale watakaofuata baadaye. Ni jambo la bahati mbaya kwamba kanuni hii imepotoshwa. Toka wakati huo, utawala wa nguvu, hiana, na kuharibu utu vimewalemea wanadamu kwa uzito. Kujiangalia nafsi kumesababisha kukubaliana na kuthaminiana kupungua. Kinachofanyiza ukristo ni kurejeza sifa za ndoa ya awali. Hisia za mume na mke zapaswa kuchangia furaha ya mwenzi. Hufanyiza umoja ambao haupotezi nafsi ya mtu ambayo ni mali ya Mungu.
Kupotoka kwenye Kanuni ya Mungu
Ndoa za mwenzi zaidi ya moja.
Utaribu wa moja kuwa na wenzi wengi ni kinyume cha umoja na upamoja ambao Mungu aliuanzisha kwenye ndoa ya kwanza. Katika ndoa yenye wenzi wengi, hakuna kuacha wenzi wengine. Kwamba Maandiko husema ndoa za Wazee wa imani zilikuwa na tabia ya wenzi wengi, maelezo yake kwa uwazi husema hazikufikia kiwango cha Mungu. Vikundi viliinuka vikihujumiana katika ndoa moja (Angalia Mwa.16; cf. 29:16, 30:24 nk.) wakitumia watoto kama zana ya kihisia kuumiza washiriki wengine wa familia. Ndoa ya mwenzi moja hujenga kumilikiana na kuaminiana kunakoimarisha kupeana haki za ndoa. Wanatambua kwamba hakuna anayeweza kushiriki kile ambacho wao wanakifurahia. Ndoa ya mwenzi moja inaakisi zaidi uhusiano wa Kristo na Kanisa na baina ya mwanadamu na Mungu.
Uasherati na uzinzi.
Mawazo ya kisasa na mazoea kwa mwanandoa huhafifisha ahadi ya uaminifu kuhusu tendo la ndoa kwa mwenzake hadi kifo. Maandiko Matakatifu huhesabu tendo la ndoa nje ya ndoa kuwa ni dhambi. Usizini (Kut.20:14). Baada ya amri hii, hakuna maelezo yanayotolewa kupinga au kutetea mazoea mabaya. Maelezo kamili ya mtazamo wa kibiblia juu ya uasherati na uzinzi hupinga uvumilivu wa kisasa wa mwenendo usiofaa kwa wanandoa wanaoridhia mambo hayo. Maelezo mengi hupinga matendo hayo. (Law.20:10-12; Mith.6:24-32; 7:6-27; 1Kor.6:9, 13, 18; Gal.5:19; Efe.5:3; 1Thes.4:3; nk.).
Uasherati na uzinzi una athari mbaya kwa mtendaji na mwanandoa aliyepunjwa haki yake, kihisia, kimwili na kifedha. Huweza kuleta magonjwa ya kuambukiza na kuzaliwa watoto nje ya ndoa. Mawingu mazito ya uwongo na kukosa uaminifu hukosesha imani ya mwanandoa mtulivu kwa mwenzake. Na huenda kukosa huko imani yawezekana isirudi. Hata kama Biblia isingekemea, matokeo mabaya ya matendo maovu yangeonya juu ya tabia hii isiyofaa.
Mawazo yasiyo safi
. Dhambi siyo kile kitendo cha nje; badala yake ni jambo linaloanzia moyoni. Yesu aliona moyo kuwa na tatizo. “Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uwongo, na matukano” (Mt.15:19). Kwa kufuatisha mtazamo huu, Yesu aliona chanzo cha kukosa uaminifu kuwa ni mawazo na hisia: “Mmesikia imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.” (Mt.5: 27-28). Wanadamu wamefungua biashara kubwa kuhusu mambo ya ngono kwa mandanguro, vitabu, Internet na video ambayo haina nafasi kwenye maisha ya kikristo. Wakristo wameitwa kuwa na mawazo safi na kuishi maisha matakatifu kwa sababu wataishi maisha matakatifu kwa umilele.
Uzinzi wa mzazi kwa mtoto wake.
Baadhi ya wazazi huvuka mipaka inayotofautisha kuonyeshana hisia za upendo kwa watoto wao kwa kuwa karibu nao kwa namna isiyostahili. Mara nyingi hili hutokea wakati uhusiano wa mume na mke unapokuwa umepuuziwa. Uchafu wa aina hii ulipigwa marufuku kwenye Agano la Kale. (Law.18:6-29; Kumb.27:20-23) na kulaaniwa kwenye Agano Jipya (1Kor.5:1-5). Jambo hili huathiri maendeleo ya mtoto na itampatia aibu siku atakayoingia kwenye ndoa. Wazazi wanapokosa kwa jambo hili humvunjia mtoto imani iliyo muhimu kwa mahusiano yake na Mungu.
Talaka.
Kauli ya Yesu hujumuisha mafundisho ya Biblia kuhusu talaka. “Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.” (Mt.19:6; Mk. 10:7-9). Ndoa ni takatifu kwa sababu Mungu ameifanya iwe hivyo. Mungu amekusudia ndoa iliyofungwa isivunjike. Alipoulizwa kuhusu amri ya Musa, Yesu alijibu kuwa ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo ila tangu mwanzo haikuwa hivyo. (Mt.19:8).
Aliendelea kusema kuwa sababu inayokubalika ya talaka ni pale mtu anapokosa uaminifu katika tendo la ndoa. (Mt.5:32; 19:9). Jibu la Yesu kwa mafarisayo linathibitisha kwamba Mungu anakusudia waliofunga ndoa kuakisi sura ya Mungu katika mwungano wa kudumu. Kukosa uaminifu kwa mwanandoa mmoja hakumaanishi lazima talaka itolewe.
Msalaba unatia moyo mtu kutubu na kusamehewa na kuondosha mizizi ya chuki. Hata kwa uzinzi, kupitia msamaha na uwezo wa Mungu wa upatanisho, mwanandoa aliyekosewa aweza kutafuta na kudumisha mpango wa asili wa Mungu. Kwa kanuni ya Biblia, uzinzi ni dhambi inayoharibu ndoa kuliko dhambi nyingine. Tunapokuwa tayari kusamehe na kuachilia hisia hasi, Mungu atakuwa tayari kuponya na kurejeza upendo kwa kila mwanandoa.
Mpango wa kimbingu kuhusu ndoa ni wa kudumu hadi kifo kitenganishe, hata hivyo wakati mwingine sheria za nchi hutoa fursa ya kutengana kutokana na ukatili kwa mwanandoa mmoja au kwa mtoto. Kutengana huko kwaweza kukawa kwa njia ya talaka tu. Kutengana huko kama haihusishi kukosa uaminifu katika tendo la ndoa, hakumpi ruhusa ya kibiblia aliyetengana kufunga ndoa nyingine. Kwa sababu ndoa ni taasisi ya kimbingu, kanisa lina jukumu kuilinda na kupinga talaka na kusaidia majeraha yake yapone kadiri inavyowezekana.
Mahusiano ya jinsia moja
Mungu aliumba mwanaume na mwanamke kutofautiana lakini kuvutiwa na kuhitaji mtu wa jinsia tofauti kwa ajili ya mahusiano yanayojenga jamii. Katika hatua nyingine, dhambi imeathiri hata jambo hili la msingi. Matokeo yake kuna mapinduzi ambayo watu wa jinsia moja huhusiana. Maandiko Matakatifu kwa nguvu nyingi hulaumu mahusiano ya jinsia moja. (Mwa.19:4-10; cf. Yud.7, 8; Law.18:22; 20:13; Rum.1:26-28; 1Tim.1:8-10). Matendo ya namna hii hupotosha sana sura ya Mungu kwa wanaume na wanawake.
Kwa sababu wote wamekosa na kupungukiwa na utukufu wa Mungu (Rum.3:23), Wakristo watashughulika ili kuwakomboa wenye mazoea ya namna hii. Watakuwa na mtazamo aliokuwa nao Yesu kwa mwanamke aliyeshikwa akizini: “Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.” (Yoh.8:11). Siyo tu kwa wenye mwelekeo wa mahusiano na wenzao wenye jinsia moja, bali wote walionaswa kwenye mazoea au mahusiano yanayosababisha mfadhaiko, aibu na kujisikia hatia huhitaji kuangaliwa na mshauri wa kikristo. Hakuna tabia iliyo ng’ambo ya uwezo wa neema ya Mungu iponyayo.
Familia
Baada ya Mungu kuwaumba Adamu na Hawa, aliwapa mamlaka ya kutawala dunia. (Mwa.1:26; 2:15). Walikuwa ni familia ya kwanza, kanisa la kwanza na ilikuwa alama ya mwanzo jamii. Kwa hiyo jamii iliundwa kwa ndoa na familia. Kwa sababu wao walikuwa ndio wanadamu wakazi pekee katika dunia, Mungu aliagiza wakazae waijaze nchi. (Mwa.1:28).
Takwimu zilizoko zadokeza kuwa sehemu ya dunia ambayo haina wakazi wanadamu haihitaji kujazwa au kutawaliwa. Lakini wanandoa wa kikristo ambao wanataka kuzaa watoto ulimwenguni wana wajibu wa kuwalea watoto wao katika njia ya BWANA, (Efe.6:4). Kabla ya wanandoa kufikiria kuzaa, wanatazamiwa kufikiri mpango wa Mungu kwa familia.
Wazazi
1. Baba.
Maandiko Matakatifu yanampa mume na baba jukumu la kuwa kiongozi na kuhani wa familia. (Kol.3:18-21; 1Pet.3:1-8). Anakuwa mfano wa Kristo, kichwa cha Kanisa. “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.
Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji na kwa neno, apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe, hujipenda mwenyewe.” (Efe.5:23-28).
Kama Kristo anavyoliongoza kanisa, mume na mke watajitoa kila moja kwa maoni ya mwenzake lakini neno la Mungu linampa upendeleo mume kwa mambo yasiyohusu dhamiri. Wakati huo huo anapaswa kuyatendea maoni binafsi ya mkewe kwa heshima. Kama Kristo alivyojitoa kwa Kanisa, vivyo hivyo mume naye anapaswa kuongoza kwa kujitoa. Kristo hulitawala Kanisa lake kwa hekima na upendo na waume nao wapaswa kutumia madaraka yao kwa upole kama Kristo anavyotumia kuongoza Kanisa.
Akiwa kuhani wa familia, Baba ataikusanya familia yake asubuhi na kuikabidhi kwa Mungu na jioni atawaongoza kumsifu Mungu na kumshukuru kwa baraka alizotoa. Ibada ya familia itakuwa kifungo kinachoifungamanisha familia – wakati unaompa Mungu kipaumbele katika familia.
Baba mwenye hekima atatumia wakati wake na watoto. Watoto waweza kujifunza mambo mengi kwa baba yao, kama kumpenda na kumheshimu mama, upendo kwa Mungu, umuhimu wa maombi, upendo kwa watu wengine, njia ya kufanya kazi, heshima ya mavazi, kupenda maumbile ya asili na vitu ambavyo Mungu amevifanya. Ikiwa baba atakosekana nyumbani, mtoto atakosa na kunyimwa fursa muhimu na furaha.
2. Mama.
Kuwa mama ni jambo la karibu zaidi duniani la kuwa mshirika wa Mungu. Mfalme aliye kwenye kiti cha enzi hana jukumu kubwa kumpita mama. Mama ni malkia nyumbani akifanyiza tabia za watoto wake kwa umilele. Anapaswa kuitazama familia kuwa ni kazi ya maisha. Jukumu la kulea watoto siyo jukumu la kumwachia mtu ambaye hana uchungu nao.
Mungu aliweka uwezo ndani ya mama, wa kumbeba mtoto ndani ya mwili wake, kumnyonyesha, kumpenda na kumhudumia hadi atakapokuwa mtu mzima. Katika nyakati za Agano la Kale, jina lilibeba kauli fupi juu ya mwenye jina. Hawa alipokea jina lake baada ya anguko dhambini. (Mwa.3:20). Kwa sababu angewazaa wanadamu wote, jina lake kiebrania chawwah lilitokna na neno kuishi (kwa kiebrania chay). Hii inaweka cheo cha mama kuwa kisicho cha kawaida katika historia ya mwanadamu.
Kama ambavyo kuzaa halikuwa jambo la Adamu peke yake wala la Hawa peke yake vivyo hivyo malezi ya watoto halikuwa jukumu la mmoja wao pekee. Kila mzazi anao wajibu na inawapasa kulea watoto katika Bwana.
Watoto
1. Kipaumbele.
Pamoja na majukumu mengine kwa Bwana, hakuna jukumu kubwa zaidi kwa wazazi linalopita la kulea watoto waliowaleta duniani. Ustawi wa watoto lapaswa kuwa jambo la kwanza badala ya kupigania maslahi binafsi. Kwa kuwa mtoto huanza kuathirika kiakili, kiroho na kimwili kabla hajazaliwa, ustawi wao wapaswa kuangaliwa kabla mama hajajifungua.
2. Upendo.
Upendo wa mzazi kwa mtoto wapaswa kuwa usio na masharti na wenye kujinyima. Hata kama hautaakisiwa, watoto lazima waupate ili waweze kujithamini, afya ya hisia katika maisha yao yote. Watoto ambao hulazimika kuuhenyea upendo wa wazazi wao hulazimika kufanya matendo mabaya yanayoweza yakawa mazoea yenye kujenga tabia. Watoto salama kwenye upendo wa wazazi wao huweza kuwafikia wengine. Waweza kufundishwa kutoa na kupokea na sababu ya kuishi kando ya kutumikia nafsi. Kadiri wanavyokua, watajifunza kumtukuza Mungu.
3. Ahadi.
Wazazi wakristo wanawajibika kuwaweka wakfu watoto wao mapema kwa kazi ya Mungu. Kanisa la Waadventista Wasabato wanayo huduma ya namna hii ambako watoto huwekwa wakfu kama Yusufu na Mariamu walivyofanya kwa mtoto Yesu. (Luk.2:22-39). Katika huduma hii, wazazi hutoa ahadi yao kumwelimisha mtoto katika njia ya Bwana ili sura ya Mungu ifanyizwe kwa mtoto. Ili kufikia lengo hili, wazazi huwajibika kuwawahisha watoto wao kwenye Shule ya Sabato na kanisani daima na kuwafanya watoto wao kuwa sehemu ya mwili wa Kristo katika umri wao mdogo.
4. Kudumu kufundisha.
Mafundisho ya kiroho ambayo wazazi hufanya kwa watoto ni mchakato unaoendelea katika kila hatua ya maisha ya mtoto. “nawe uwafundishe watoto wakokwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako (Kumb.6:7-9; 11:18). Mivuto ya kiroho ya mtoto hufanyizwa kwa kila mazingira ya nyumbani wala siyo ibada peke yake. Itawafikia katika kumtumainia Yesu, katika mitindo yao ya maisha, mavazi, na mapambo ya nyumbani. Kumjua Mungu kama mzazi apendaye ni muhimu kwa maisha ya kikristo ya mtoto.
5. Kujifunza utiii.
“Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa Mzee.” Nidhamu ina maana pana kupita adhabu. Adhabu mara nyingi hushughulikia yaliyopita wakati nidhamu hutazama yajayo mbele. Kwenye nidhamu, mchakato humfanya mtoto awe mfuasi wa mzazi kwa ajili ya kujifunza, uongozi, na mfano wa kuiga. Humaanisha kufundisha kanuni muhimu kama utii, ukweli, haki, msimamo, uvumilivu, utaratibu, rehema, ukarimu na kutenda kazi.
Mtoto akijifunza kuwatii wazazi wake tangu udogoni, mamlaka haitakuwa jambo lenye kumsumbua kwenye maisha yake. Aina ya utii ajifunzayo mtoto ni muhimu kwa kuwa utii wa kweli huwa unafanywa siyo kwa sababu tu unatakiwa bali pia kwa sababu ni jambo linatoka moyoni. Siri ya utii wa aina hii inabeba kuzaliwa upya.
Mwanadamu anayejaribu kutii amri za Mungu kwa sababu ni wajibu, kwa sababu tu anatakiwa kufanya hivyo hataingia kwenye raha ya kutii. Utii wa kweli kunatokana na kanuni itendayo kazi kutoka moyoni. Inatokana na kupenda haki, upendo wa sheria ya Mungu. Kinachofanyiza haki ni utii kwa Mkombozi wetu. Hili hutuongoza kutenda haki kwa sababu ni vema, kwa sababu haki humpendeza Mungu.
6. Kuingia kwenye jamii na kujifunza Lugha.
Katika familia, watoto huingia kwenye jamii kama washirika wa wanadamu pamoja na majukumu yote na fursa zinazohusika. Kushirikiana ni mchakato ambao mtoto huingia ili atumikie jamii. Lugha pamoja na yahusuyo kuwasiliana ni ujuzi wa kwanza ambao mtoto hujifunza. Lugha itumikayo nyumbani yahitaji uangalizi makini, ili hatimaye imtukuze Mungu. Mtoto apaswa kusikia mara kwa mara maelezo ya furaha kwa wanafamilia na sifa kwa Mungu.
7. Kutambua jinsia.
Nyumbani, kutokana na kutenda kazi kwa wanaume na wanawake wafanyao mfumo wote wa familia, watoto hujifunza kutenda kama wanaume na wanawake ndani ya jamii. Wazazi wapaswa kuwafundisha maendeleo yao ya kijinsia kwa kuwapatia habari sahihi. Ni jukumu la wazazi pia kuwalinda watoto na matumizi mabaya ya viungo vya uzazi.
8. Kujifunza mema.
Jambo la msingi analojifunza mtoto katika kufanya ushirika na jamii ni kuzijua na kuzifuata kanuni za wema zinayothaminiwa na familia. Kile familia kinachothamini na dini huwa vinaweza kutofautiana. Wazazi wanaweza kudai kuthamini mambo kadhaa ya maisha lakini kanuni wanazoishi kwazo zikawa hazifuatishi kile wanachosema. Ni muhimu wazazi kuzingatia kutokutoa ujumbe unaogongana kwa watoto.
Familia Pana (kubwa).
Ndoa kama Mungu alivyoikusudia hutenga watu wengine, lakini familia hapana. Katika ulimwengu tulio nao ni vigumu kupata familia pana, kwamba yupo babu na bibi, ndugu wa baba wengine, wajomba na binamu kwa ukaribu. Kanisa laweza kuwapatia wale ambao mbali kupata ufahamu wa kujithamini na watu wanaoweza kuwategemea. Hapa pia mzazi moja atapata mahali pa kulea mtoto wake. Kanisa laweza kutoa vielelezo visivyopatikana nyumbani.
Kupitia kuwapenda wenye umri mkubwa walioko kwenye mkutaniko wa kanisa, watoto watajifunza kuheshimu. Wazee nao wataridhika kupata watoto wa kuwapenda na kuwafurahia. “Na hata nikiwa mzee mwenye mvi, Ee Mungu usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako. Na kila atakayekuja uweza wako.” (Zab.71:18).
Mungu hufikiria wazee kwa namna ya pekee, akisema, “Kichwa chenye mvi ni taji ya utukufu, kama kikionekana katika njia ya haki.” (Mith.16:31). Pia, “na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa.” (Isa.46:4).
Katika Kanisa, waseja watapata fursa ya kupendwa na kufurahiwa na kushiriki nguvu zao pia. Kupitia huduma yake, watatambua upendo wa Mungu kwao: “Naam, nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.” (Yer.31:3).
Ni sehemu ya “dini safi” kuangalia kwa namna ya pekee wanaohitaji msaada. (Yak.1:27; Kut. 22:22; Kumb.24:17; 26:12; Mith.23:10; Isa.1:17). Familia ya Kanisa inayo fursa kutoa kituo cha pumziko, hifadhi, mahali pa kuthaminiwa kwa wale wasio na familia; itamzingira kila mshiriki kwa umoja wa kipekee ambao Kristo alisema ndio utakaotambulisha ukristo wenyewe. (Yoh.17:20-23).


