Utangulizi
Kwa maelfu ya miaka, Sanduku la Agano limekuwa moja ya tunu za muhimu sana katika historia ya Biblia. Je, sanduku hili takatifu, ambalo lilihifadhi Amri Kumi, litaonekana tena mbeleni au limepotea milele? Je, kuna wakati Mungu ataliweka wazi ili lionekane tena kwa ulimwengu? Makala hii inaangazia kile ambacho Ellen G. White anasema kuhusu mada hii. Makala hii inaeleza uwepo wa Sanduku la Agano la mbinguni, na jinsi lile la duniani lilivyofichwa. Nini kitatokea baadaye kuhusu sanduku hili la Agano? Ndio kusudi hasa la makala hii.
Agano na Sanduku la Agano
Agano kama agano ni makubaliano. Agano kati ya Mungu na Israeli yalikuwa makubalino ambayo pande zote mbili ziliingia, katika maagano hayo Waisraeli walipaswa kuwa watu Wake, kumtii na kuwa wawakilishi Wake kwa ulimwengu, na ambapo Mungu, kwa upande Wake, angewabariki na kuwa Mungu wao (tazama Kut. 19:5 na 24:7). Ilikuwa katika misingi ya uamuzi wao wa hiari wa kukubali jukumu la kuwa watu wa Mungu waliochaguliwa ndipo aliwapa Amri Kumi, ambazo waliahidi kuzitii kama sehemu yao ya makubaliano (Kut. 19:8; 24:3, 7). Kwa hivyo, Amri Kumi, zilizoandikwa kwa mkono wa Mungu juu ya mbao mbili za mawe, ziliitwa “agano” (Kumb. 4:13), kwa kuwa zilikuwa nakala iliyoandikwa ya masharti ya msingi wa agano hilo. Sanduku lenyewe, lililokuwa na Amri Kumi, kwa hivyo, likawa likijulikana kama “sanduku la agano” (tazama Kut. 25:16 na Hes. 1:50). -- Francis D. Nichol, mhariri, The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, juzuu ya 1 (Review and Herald Publishing Association, 1978), ukurasa wa 855–857.
Sanduku la Agano lilikuwa kifaa muhimu zaidi miongoni mwa vyombo vyote vilivyokuwemo katika hema ya kukutania, moyo wa patakatifu, msingi wa agano (Kumb. 4:12, 13), na mahali pa uwepo wa Mungu miongoni mwa watu Wake (tazama Kut. 25:8, 21, 22). -- Francis D. Nichol, mhariri, The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, Vol. 1 (Review and Herald Publishing Association, 1978), Pg. 688.
Amri Kumi Katika Hekalu la Mbinguni
Ellen G. White anaeleza kuwa Amri Kumi ziliwekwa kwenye Sanduku la Agano katika patakatifu pa mbinguni na duniani:
- “Huko nililiona sanduku... Ndani ya sanduku kulikuwa na mbao za mawe zenye Amri Kumi.” (EW 251, 252)
- “Yesu alifunua kifuniko cha sanduku, nami nikaona mbao za mawe zilizoandikwa Amri Kumi.” (LS 95)
- “Katika hekalu la mbinguni, katika makao ya Mungu, kiti Chake cha enzi kimesimikwa katika haki na hukumu. Katika Patakatifu pa Patakatifu imo sheria Yake, kanuni kuu ya haki ambayo wanadamu wote wanapimwa kwayo. Sanduku linalohifadhi mbao za sheria limefunikwa kwa kiti cha rehema, ambacho mbele yake Kristo huwasilisha damu Yake kwa ajili ya mwenye dhambi.” (GC 415)
Sheria ya Asili Iliyopo Mbinguni
Ellen White anaeleza kuwa mbinguni iko sheria halisi, na kwamba hapa duniani kuna nakala yake ambayo sasa ndiyo iliyoandikwa katika zile mbao mbili za mawe:
- Watu wenye “Akili na mioyo yenye kuasi wamewahi kufikiri kuwa walikuwa na nguvu ya kutosha kubadilisha nyakati na sheria za Yehova; lakini, salama katika kumbukumbu za mbinguni, katika sanduku la Mungu, ziko nakala halisi za amri za Mungu, zilizoandikwa juu ya mbao mbili za mawe. Hakuna mamlaka duniani iliyo na uwezo wa kuzitoa mbao hizo kutoka mahali pake patakatifu pa maficho chini ya kiti cha rehema.” (ST February 28, 1878, par. 10)
- “Sheria ya Mungu katika hekalu la mbinguni ndiyo ile ya asili (original), ambapo Amri zilizoandikwa katika mawe… zilikuwa nakala sahihi kabisa.” (GC 434)
Sanduku la Agano la Duniani Lililofichwa
Kabla hekalu la Yerusalemu halijaharibiwa katika mwaka 70 B.K., watu wa Mungu walilichukua lile Sanduku la Agano na wakalificha ili lisije likaanguka katika mikono ya adui:
- “Watu waaminifu… waliliondoa sanduku lililokuwa na mbao za mawe, na… wakalificha katika pango… Sanduku hilo bado limefichwa.” (4SG 114, 115)
- “Kwa huzuni na machozi walilificha sanduku hilo ndani ya pango… Halijawahi kuguswa tangu lilipofichwa.” (PK 453)
Ufunuo wa Baadaye
Nabii anaendelea kueleza kuwa wakati flani Mungu atazifunua tena Amri Kumi na kuzifanya zieonekane:
- “Katika wakati uliopangwa na Mungu, Atazileta mbao hizi za mawe kuwa ushahidi kwa dunia nzima.” (Ms 122, 1901)
- “Wakati hukumu itakapoketi… ndipo mbao za mawe, zilizofichwa na Mungu mpaka siku hiyo, zitaonyeshwa hadharani kama kigezo cha haki.” (RH Januari 28, 1909)
Matukio Mawili ya Ufunuo
White anaeleza kuwa Amri Kumi zitaonekana kwa ulimwengu katika nyakati mbili:
- Kabla ya Kurudi kwa Yesu:
- “Utukufu wa mji wa mbinguni unamiminika kutoka katika malango yaliyo wazi. Kisha, mkono unaoshikilia mbao mbili za mawe zilizounganishwa pamoja unaonekana angani. Nabii asema: "Mbingu zitatangaza haki yake, kwa maana Mungu ndiye hakimu mwenyewe." Zaburi 50:6. Sheria hiyo takatifu, haki ya Mungu, ambayo ilitangazwa kutoka Sinai katikati ya radi na moto kama mwongozo wa maisha, sasa inafunuliwa kwa wanadamu kama kanuni ya hukumu. Mkono unazifungua mbao hizo, na hapo zinaonekana amri zile kumi, zilizoandikwa kana kwamba kwa kalamu ya moto. Maneno yake yako wazi kiasi kwamba wote wanaweza kuyasoma. Kumbukumbu zinaamshwa, giza la ushirikina na uzushi linafutwa kutoka katika kila akili, na maneno kumi ya Mungu—mafupi, yanayojitosheleza, na yenye mamlaka—yanawasilishwa mbele ya macho ya wakazi wote wa dunia.” (GC 639)
- Wakati wa Utukufu wa Mwisho wa Kristo: Akieleza namna kutukuzwa kwa mwisho kwa Kristo na hukumu ya mwisho ya wanadamu itakavyokuwa mwishoni mwa milenia, Ellen White anasema:
- “Wataona mikononi Mwake meza za sheria ya kiungu, sheria ambazo walizidharau na kuzivunja.” (GC 668, 669)
Hitimisho
Sanduku la Agano linabeba umuhimu mkubwa wa kihistoria na wa kiroho. Ingawa limefichwa kwa sasa, maandiko yanaonyesha kuwa Mungu atalifunua tena kwa dunia, likiwa ushuhuda wa sheria Yake ya milele. Kwa hivyo, swali si
ikiwa Sanduku la Agano litaonekana tena, bali
lini Mungu atalifunua kwa ulimwengu wote.